Rais William Samoei Ruto, ametangaza rasmi kuwa kuanzia mwaka huu, tarehe 27 Agosti ya kila mwaka itaadhimishwa kama “Katiba Day” (Siku ya Katiba]
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Siku ya Katiba ni kwa heshima ya kutangazwa kwa Katiba ya Kenya ya mwaka 2010, ambayo iliidhinishwa rasmi mnamo 27 Agosti 2010, chini ya uongozi wa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu, Hayati Mwai Kibaki
Katika tangazo hilo, Rais Ruto alieleza kuwa Siku ya Katiba itaadhimishwa katika kila pembe ya Jamhuri ya Kenya pamoja na balozi zote za Kenya nje ya nchi. Akisema kuwa lengo kuu la siku hiyo ni Kufufua na kuimarisha mshikamano wa pamoja katika kulinda na kutekeleza maadili ya Katiba, kuendeleza mazungumzo ya kitaifa kuhusu utawala wa kikatiba, na kuhimiza utiifu kwa misingi ya sheria.
Aidha amesema kwamba siku hii itakuwa siku ya kazi, lakini taasisi zote za serikali katika mihimili mitatu ya utawala yaani Bunge, Mahakama, na Serikali Kuu pamoja na ngazi zote mbili za utawala (Serikali Kuu na Serikali za Kaunti), zinapaswa kuandaa na kushiriki katika shughuli za kijamii zenye mwelekeo wa uelimishaji wa Katiba.
Rais Ruto alieleza kuwa siku hiyo ni nafasi muhimu kwa shule, vyuo, taasisi za kiraia, viongozi wa kisiasa, na wananchi wote kwa ujumla kushiriki katika mijadala ya kikatiba, midahalo, maonyesho ya elimu ya uraia, na shughuli nyingine za kuongeza uelewa kuhusu Katiba na haki za kikatiba.
“Taasisi zote za serikali katika mihimili mitatu ya utawala, na katika ngazi zote mbili za uongozi, zikiwemo shule, zitatakiwa kuandaa, kuendesha na kushiriki katika shughuli za kiraia zenye uzito na heshima katika siku hiyo ili kuhamasisha uelewa wa Katiba na ushiriki wa raia katika masuala ya kikatiba”ilinukuu sehemu ya ujumbe huo



