Ni Vita Dhidi Ya Ufisadi, Ama Ni Sarakasi Za Kisiasa?

0
116
PICHA /Rais William Ruto

Katika hatua mpya ya kupambana na ufisadi, serikali ilitangaza kuundwa kwa Kikosi Kazi Jumuishi (Multi-Agency Team – MAT), kitakachojumuisha taasisi mbalimbali za serikali, sekta binafsi, na mashirika ya kimataifa. Kikosi hiki kimepewa majukumu makubwa: kusimamia, kuratibu na kuimarisha vita dhidi ya ufisadi, utakatishaji wa fedha na uhalifu wa kiuchumi. Ingawa nia hii inaonekana kuwa njema, kuna maswali halali yanayoibuka kutoka kwa wananchi je, hii ni hatua ya kweli ya mageuzi, au ni sarakasi nyingine ya kisiasa iliyojaa porojo na matumizi yasiyo na tija ya fedha za umma?

MAT inajumuisha taasisi nyeti kama Ofisi ya Rais, EACC, DCI, ODPP, KRA, CBK na nyinginezo. Hizi ni taasisi ambazo tayari zina dhamana ya kushughulikia ufisadi, lakini hazijawahi kuwiana na matarajio ya wananchi kwa muda mrefu. Katika historia ya hivi karibuni, tumeona kesi nyingi kubwa za ufisadi zikikamatwa kwenye vichwa vya habari lakini zikizama kimya kimya mahakamani zikipotea kwa hila, ucheleweshaji, au ushawishi wa kisiasa.

Acha niseme hivi,tatizo si ukosefu wa taasisi, bali ni uhuru na dhamira ya kweli ya utendaji. Kama taasisi hizi zimekuwa zikishindwa kufanya kazi zikiwa peke yao, ni nini kinachotuhakikishia kuwa zikiunganishwa chini ya mwavuli mmoja, zitaweza kuleta mabadiliko ya kweli? Zaidi ya hayo, kikosi hiki kinasimamiwa moja kwa moja kutoka kwa Ofisi ya Rais jambo linalozua hofu kuhusu uhuru wake, hasa ikizingatiwa kuwa baadhi ya wanasiasa wakuu wamewahi kutajwa katika kashfa mbalimbali bila kuchukuliwa hatua.

Pia kuna swali kuhusu rasilimali: Rais ametangaza kuwa MAT itagharimiwa kupitia bajeti za kawaida za taasisi shiriki, huku serikali ikitoa msaada wa ziada pale inapohitajika. Hii ni hatari iwapo matumizi haya hayatawekewa uwazi na ukaguzi wa kina. Kwa maneno mengine, huenda pesa za mlipa kodi zikatumika kufadhili kampeni za kisiasa zilizo kwenye mwavuli wa “vita dhidi ya ufisadi”.

Swali kuu ni mashirika haya yanawezaje kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi ikiwa hayako huru? Na je, kuna vipengele vya kikatiba au vya kisheria vinavyowakinga wahusika wakuu wa ufisadi kiasi cha kuzuia hatua kuchukuliwa dhidi yao? Kama vipo, basi mapambano haya hayawezi kuzaa matunda bila marekebisho ya kisheria na kisera.
Mwisho wa siku, wananchi hawahitaji miungano ya kisiasa ndani ya majina ya vikosi kazi; wanahitaji hatua za kweli, haki isiyoegemea upande wowote, na uwajibikaji usio na mapendeleo.

Kama MAT haitakuwa huru, haitakuwa wazi, na haitakuwa na dhamira ya kweli — basi haitakuwa chochote zaidi ya jukwaa la PR linalowatumbukiza wananchi katika mzigo wa matumizi bila matumaini ya haki.

 

LEAVE A REPLY