Wahadhiri Wa Chuo Kikuu Cha Moi Watoa Ilani Ya Mgomo Wa Siku Saba

0
126
wahadhiri wa chuo kikuu cha moi wakindamana katika picha ya awali

Chama cha Wahadhiri wa Vyuo Vikuu nchini (UASU) kimetoa  ilani ya mgomo wa siku saba kwa Chuo Kikuu cha Moi kikilalamikia kucheleweshwa kwa mishahara pamoja na kutotekelezwa kwa makubaliano yaliyofikiwa awali.

Katika taarifa iliyotolewa tarehe 12 Agosti, Katibu Mkuu wa UASU, Constantine Opiyo, alisema kuwa wanachama wote wa chama hicho katika Chuo Kikuu cha Moi watasitisha kazi kuanzia tarehe 20 Agosti 2025, hadi pale mkataba wa kurejea kazini utakapotekelezwa kikamilifu.

Chama   hicho sasa kinataka mishahara ya miezi ya Juni na Julai 2025 ilipwe kulingana na viwango vya makubaliano ya pamoja ya mwaka 2021-2025

Vilevile, UASU inasisitiza kuwa makubaliano yaliyotiwa saini kati ya chama hicho na Baraza la Chuo tarehe 30 Novemba 2024 yaheshimiwe. Pia, wanataka vipengele vinavyohusu kupandishwa vyeo kwa watumishi na umri wa kustaafu vilivyomo katika makubaliano ya kitaifa ya 2021-2025 vizingatiwe kikamilifu.
Kwa muda mrefu sasa, Chuo Kikuu cha Moi kimekumbwa na matatizo ya kiutawala yaliyopelekea kupotea kwa fedha, migomo ya mara kwa mara, na hali ya kukatisha tamaa kwa wanafunzi na wazazi.

Mnamo Januari mwaka huu, Waziri wa Elimu Julius Ogamba alizindua baraza jipya la chuo hicho akisema kuwa serikali ililazimika kuchukua hatua madhubuti kwa kulivunja baraza la awali lililosababisha kudorora kwa usimamizi wa taasisi hiyo.

Waziri Ogamba alisema hatua hiyo inalenga kurejesha hali ya utulivu na mwelekeo sahihi wa masomo chuoni humo baada ya kipindi kirefu cha msukosuko ya uongozi.

LEAVE A REPLY