Dawa za Kulevya ni Janga la Dharura

0
96

Ama kweli, dawa za kulevya ni janga kubwa ambalo limekuwa likiisumbua nchi kwa muda mrefu sasa. Madhara yake ni mengi na yanajulikana bayana vijana kupotea, familia kusambaratika, uhalifu kuongezeka na maendeleo kurudishwa nyuma. Taifa haliwezi kusonga mbele wakati kizazi chake kinaangamizwa na sumu.

Hivi majuzi, Rais William Ruto ametangaza waziwazi vita dhidi ya dawa za kulevya. Kauli yake imeleta matumaini mapya kwa Wakenya wengi waliokata tamaa. Rais ameahidi kuwa wale wote watakaopatikana wakijihusisha na biashara au usambazaji wa dawa za kulevya watakumbana na mkono mrefu wa sheria, bila kujali cheo au hadhi yao katika jamii.

Zaidi ya hayo, Rais amesema kuwa serikali iko mbioni kupeleka mswada bungeni utakaolenga kupitisha sheria kali ikiwemo adhabu ya kunyongwa kwa wahusika wakuu wa dawa hatari kama cocaine na heroin. Hii ni hatua nzito, lakini ni hatua inayolingana na ukubwa wa janga tunalokabiliana nalo.

Hata hivyo, kauli na ahadi hazitoshi. Ikiwa Rais ana ndoto ya kweli ya kuikomboa nchi dhidi ya dawa za kulevya, basi tunataka kuona sheria ikitekelezwa bila ubaguzi. Wafanyabiashara wakubwa, vigogo wa kisiasa, maafisa serikalini, na matajiri wanaolindwa kwa nguvu za pesa lazima wachukuliwe hatua kali kama raia wa kawaida. Haki ikibagua, basi vita hii itakuwa porojo tu.

Dawa za kulevya zinarudisha maendeleo nyuma. Hakuna uchumi unaoweza kukua wakati vijana wake ni waraibu hakuna usalama bila nidhamu na hakuna mustakabali bila kulinda kizazi kijacho.

LEAVE A REPLY